Excerpt for Simulizi Ya Dunia Kwa Kugeza Tanzania by , available in its entirety at Smashwords

Simulizi ya Dunia
Kwa Kugeza Tanzania


Simulizi ya Dunia
Kwa Kugeza Tanzania

Omari Rashid Nundu

Dibaji

Dunia ni kubwa na kuivinjari ni muhimu kwa atakayejaliwa uwezo wa kufanya hivyo. Somo la Jiografia linatowa mwanga huo mashuleni; pia uelewa wa mtu kuhusu Dunia unaimarishwa na utafiti wake mwenyewe kwa mambo anayoyaona na vitu anavyochezea akiwa mdogo. Udogoni nilibahatika kuishi mjini na vijijini nikicheza nchi kavu na hata mitoni na baharini. Maajabu yaliyoko huku ni mengi. Masomo ya shuleni na vyuo vikuu ndiyo hasa yanayafunua macho ya mweledi akayaelewa yale aliyoamua kuyasomea. Nilipenda sana kurusha tiara nilizozitengeneza mwenyewe. Kuunda na kuchezea tiara havikunitosha. Nilinuwia na nikajaaliwa kusomea fani ya uhandisi wa vyombo virukavyo angani. Hakuna jambo ambalo liliburudisha akili na mawazo yangu kama kujifunza, kudadisi na kutafiti kwa kina maswala haya. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kuniongoza huko. Maisha yangu yote ya udogoni na ukubwani yalitumika kwenye nyanja zihusuzo mambo hayo.

“Kila mtu ana ulevi wake” ndivyo Waswahili tusemavyo nao wangu ulikuwa ni kusoma na kutunga mashairi. Sikuhitaji kufundishwa kufanya hivyo. Ni wazi kuwa mapenzi ya nyimbo za taarab yalinirahisishia kukitiza akilini mwangu vina na mizani kwa sentenso nizisemazo kila nilipotaka kufanya hivyo, na ndio maana niliweza kutunga mashairi na kuyatuma kwenye magazeti ya Ngurumo na Mwangaza nikiwa mdogo sana, mara tu baada ya kuanza kwenda shule. Katika harakati za kutafuta uhuru wa Tanganyika, mwanasiasa mmoja alipopinga ushiriki wa ubunge uliotaka kuwepo wabunge watatu kila jimbo kwa kuzingatia rangi yaani Mwafrika, Mhindi na Mzungu nilijikuta kukubaliana na wale walioafiki mfumo huo na nikatunga na kutuma shairi gazetini kumlaumu yule aliyepinga. Mtu huyu ambaye alikuwa mwanachama wa chama cha siasa cha TANU ilimbidi aanzishe chama chake. Wakati mwengine najiuliza kwanini nilifanya hivyo bali sipati jibu la kuniridhisha. Hadi leo bado nashangaa kwanini nilifanya hivyo. Siamini kuwa upeo wa kisiasa wa umri wangu mdogo ule ulikuwa mkubwa kuliko wa ukubwani huu. Hata hivyo apangae na aongozaye ni Mwenyezi Mungu; basi naiwe hivyo.

Hadi ukubwani nilipotamani kufanya jambo la kuniburudisha kutunga shairi kulijitokeza. Nilifanya hivyo sana nilipokuwa kwenye Jeshi la Kujenga Taifa, Ruvu, Disemba 1970 ambako nilitunga ngonjera kwa mashindano ya Wilaya ya Bagamoyo hadi Jimbo la Mashariki la wakati huo. Ngonjera yangu ndiyo iliyotumika kumsomea Mwalim Julius Nyerere wakati wa kutufungia mafunzo. Sikuisoma mimi.

Mimi ni Muhandisi aliyebobea kwenye vyombo vya anga. Hivyo nilitumia miaka mingi ya maisha yangu ndani na nje ya Tanzania kwenye taasisi na mashirika ya usafiri wa anga. Baada ya kujishughulisha na mambo mengi ya kuendeleza nchi yangu, nchi za Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Africa (SADC), Afrika na Dunia nzima kwa jumla, shughuli ambazo ziliniwezesha kutembelea na pia kujifunza na kufanya kazi nchi nyingi duniani, mwaka 2010 nilirejea nyumbani kwetu Tanzania nikiwa na nia ya kupata nafasi ya kuwa mwakilishi wa wilaya yangu ya Tanga bungeni na hivyo basi kuweza kuchangia kwa dhati katika maendeleo ya nchi yangu kwa kutumia kikamilifu elimu na uzoefu nilioupata ndani na nje ya nchi yangu. Nilibahatika kuwa mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; hali kadhalika nikawa waziri wa Wizara mpya ya Uchukuzi. Hii ilikuwa nafasi nzuri iliyoje kwa mimi kujitolea na kujumuika kikamilifu katika kuchangia kuijenga nchi yangu hasa ikizingatiwa kuwa taasisi muhimu nyingi za wizara hiyo zilikuwa zimekufa kabisa au zilikuwa zinasuasua. Nilidhamiria kuziuisha na kuzijenga taasisi hizi pamoja na kupambana na kusambaratisha aina yoyote iwayo ya rushwa ambayo ingejitokeza. Sikuchelea kuwaeleza watendaji hivyo nikitegemea kuwa wangeniunga mkono kwenye azima hii. Shirika la Ndege ambalo nililitumikia katika ujana wangu pamoja na kuliunda na kulijengea miundombinu yake na kushiriki kwenye mipango na utekelezaji wa nyenzo zake kubwa zikiwemo ndege nililikuta lina ndege moja tu ambayo haikuwa inaruka bali ilikuwa matengezoni. Karakana kubwa ya ndege ambayo ujenzi wake niliusimamia mimi mwenyewe hadi ikaanza kutumika niliikuta imegeuzwa gofu lisilousishwa na utengenezaji wa ndege kabisa. Shirika la Reli lililokuwa limewekwa kwenye ubia lilikuwa linafanya vibaya sana, na ilinichukuwa miezi minane kuuvunja ubia huo. Bandari nazo zilikuwa hoi. Kwa muda mfupi wa mwaka mmoja na nusu niliokuwa waziri katika wizara hiyo niliona mengi, nilijifunza na kuelewa matatizo mengi zaidi ya nilivyotarajia.

Utenzi huu ni simulizi ya niliyoyaona tangu udogoni mwangu hadi mwaka 2015 nilipouandika. Lengo kubwa ni kumburudisha msomaji na kumfundisha mwanafunzi wa lugha ya Kiswahili. Burudani iliyomo ndani ya lugha ya Kiswahili inatokana na utamu wa maneno yenye maana ya ndani sana na yanayompa mshairi fursa ya kuyapanga na kuyakusanya atakavyo akijieleza kwa ufasaha.

Vilevile utenzi huu ni mkusanyiko wa mambo mengi ya Dunia hii na mwenendo wa Tanzania ndani yake ambayo nimeazimia kuyasimulia. Ni mategemeo yangu kuwa yaliyomo humu yataburudisha kiutenzi na kiushahiri na pia yatachangamsha mawazo ya msomaji katika kufikiria hali ya Tanzania na nafasi yake katika wigo wa uchumi wa Dunia katika kipindi hiki cha mwanzo wa karne ya ishirini na moja.

Nimechagua Tanzania kwa kuwa ni kwetu lakini kuna nchi nyingi za Kiafrika na kwengineko ambazo zinawasilishwa kwenye simulizi hii. Nimeandika kwa sababu nina mapenzi ya dhati kwa nchi yangu na pia nina imani kubwa kuwa Tanzania inayo nafasi ya kuibuka kuwa moja ya nchi tajiri sana duniani kama hatua kabambe zipasazo za kupambana na matatizo ya rushwa, uonevu, umbea, usaliti, unafiki, chuki, madawa ya kulevya na ubadhirifu wa rasilimali zitachukuliwa hivi sasa bila kusubiri zaidi. Vinginevyo Tanzania itabakia kuonekana masikini daima ingawa ina rasilimali zote zinazohitajika kuondokana na balaa hili. Rasilimali watu ikibadilika na kuamua kwa dhati kupambana na matatizo yaliyopo nchi itaendelea kwa kasi sana kwa faida ya kila mwananchi.

Wakati unaburudika na utenzi huu pia itafakari sana hatima ya Tanzania.

Omari Rashid Nundu

15 Mei 2015

Copyright © 2017 Omari Rashid NunduPublished by Omari Rashid Nundu Publishing at SmashwordsFirst edition 2017All rights reserved. No part of this book may be reproduced or transmitted in any form or by any means, electronic or mechanical, including photocopying, recording or any information storage or retrieval system without permission from the copyright holder.The Author has made every effort to trace and acknowledge sources/resources/individuals. In the event that any images/information have been incorrectly attributed or credited, the Author will be pleased to rectify these omissions at the earliest opportunity.Hatimiliki © 2017 Omari Rashid NunduToleo la kwanza 2017Haki zote zimehifadhiwa. Hairuhusiwi kuchapisha au kusambaza sehemu yoyote ya kitabu hiki kwa njia yoyote iwayo, si ya elektroniki wala ya mitambo, kwa kufotokopi, kurekodi au kuhifadhi kwa kuitumia baadaye bila ya idhini ya mwenye hatimiliki.Mwandishi amefanya juhudi zote kufuatilia na kutambua vyanzo vyote na ikitokea kuwa vyanzo vya picha au habari havikutambuliwa ipasavyo, Mwandishi atafurahi kurekebisha upungufu huo mapema iwezekanavyo.

ORODHA YA YALIYOMO

Dibaji

I. Utangulizi

II. Maudhui ya Dunia

III. Taswira ya Ulimwengu

IV . Mwenendo wa Dunia

V. Misingi ya Ufanisi – Upendo

VI. Misingi ya Ufanisi – Elimu

VII. Misingi ya Ufanisi – Nyenzo na Shughuli

VIII. Misingi ya Ufanisi – Uchukuzi

IX. Misingi ya Ufanisi – Afya

X. Kipimo cha Ufanisi – Thamani ya Utu

XI. Haki na Sheria

XII. Upotovu na Utovu wa Sheria

XIII. Uchumi na Wananchi

XIV. Busara na Uongozi

XV. Nasaha za Utenzi

XVI. Hitimisho na Shukran

Msamiati

I. Utangulizi

1

Ninaishika kalamu,

Kwani moyo una hamu,

Kuwataka mfahamu,

Haya nilokusudia.2

Napuliza baragumu,

Mnisikize kaumu,

Naanza kuwasalimu,

Niyakidhi mazoea.3

Mkishajibu salamu,

Mbakie mumu humu,

Ninayo mambo muhimu,

Nataka wahadithia.4

Ni mengi niliyonayo,

Yamejaa kwenye moyo,

Ni mambo twaishi nayo,

Ni vyema kuyatambua.5

Kila mara ninawaza,

Kama nitawaliwaza,

Nisiwe wakuwakwaza,

Muishie kunizia.

6

Nia mbaya kwenu sina,

Naweka mambo bayana,

Tuweze kuelewana,

Tuachane na hisia.7

Mniombeeni sana,

Kwa jambo hili kufana,

Ni kitendo cha maana,

Nilichokinuwilia.8

Vile mkiniombea,

Na mimi nawaombea,

Sote tupate shufaa,

Lengo lipatetimia.9

Nawaombea kwa Bwana,

Mtukufu wa mabwana,

Mfano wake hakuna,

Kila mja atambua.10

Yeye tusimkufuru,

Tufwate aloamuru,

Apate kutunusuru,

Siku itapowadia.

11

Nilipo natetemeka,

Nisije nikaropoka,

Naogopa kudhurika,

Mola asiporidhia.12

Namuomba Mola wangu,

Yeye ni Mwenyezi Mungu,

Nampa maombi yangu,

Uamuzi namwachia.13

Nawarehemu wazazi,

Vilevile na walezi,

Peponi kuwa fauzi,

Ndivyo navyowaombea.14

Wengi ninawashukuru,

Kwa walivyo ninusuru,

Sitowataja kwa duru,

Wengine sijesalia.15

Shukrani za jumla,

Ki desturi na mila,

Walipo kila mahala,

Ziweze kuwafikia.

16

Wote ninawathamini,

Kwa yao kubwa imani,

Niliwachwa ukembeni,

Na wao wakanilea.17

Walinifunza walimu,

Kwa wao utaalamu,

Mafunzo nilohitimu,

Yote nayazingatia.18

Nitawapa kitu gani,

Ili kiweze baini,

Uzito wa shukrani,

Ninazozikusudia.19

Nipande majukwaani,

Nitangaze hadharani,

Niishi nao nyumbani,

Deni halitapungua.

II. Maudhui ya Dunia

20

Baada kusema haya,

Najuwa mmengojeya,

Sasa basi ninauya,

Kuwelezea Dunia.21

Naongelea Dunia,

Mungu alotuumbia,

Nyenzo akatuwekea,

Tuweze kuzitumia.22

Dunia ina milima,

Mirefu imesimama,

Ilipo haitahama,

Achilia kusogea.23

Duniani kuna maji,

Shambani na kwenye miji,

Kaziye kutufariji,

Kiu kinaposumbua.24

Kila kitu kina maji,

Hakuna atayehoji,

Yapo kwenye kila mji,

Baharini yamejaa.

25

Maji kwetu yana tija,

Huzikidhi zetu haja,

Huyanywa tukiyachuja,

Na pia kusafishia.26

Maji ndiyo yalo mengi,

Yameenea kwa wingi,

Ni asilimia nyingi,

Kwa kila kinopumua.27

Mili yetu ina maji,

Yatokanavyo vinywaji,

Huwa damu haivuji,

Yalinda na kukagua.28

Mvua ikibubujika,

Mito nayo hufurika,

Ikizidi ni gharika,

Balaa imeingia.29

Mvua tunazozitaka,

Ni za Vuli na Masika,

Kwazo huwa twaridhika,

Mashamba kuyaandaa.

30

Ni mvua zenye baraka,

Tupandiazo nafaka,

Si mvua zenye wahaka,

Mafuriko kutokea.31

Mazao yakipevuka,

Twavuna kwa uhakika,

Tunauza na kupika,

Na mengine husalia.32

Kwenye bahari na mito,

Maji yapoleza joto,

Na kuondoa fukuto,

Ambalo linasumbua.33

Siku mvua inyeshapo,

Ukawa upapo hapo,

Utakutesa upepo,

Na mwilio utaroa.34

Upepo huvuma mno,

Sauti ya mnong’ono,

Kiusaka kuuono,

Bali utausikia.

35

Unavyotikisa miti,

Ikayonga kama njiti,

Nguvuze ni madhubuti,

Si kitu cha kuchezea.36

Baharini hucharuka,

Meli zikakokoteka,

Mawimbi hubabaika,

Huibuka na kunywea.37

Nyumba zinatetemeka,

Na mapaa kufumka,

Vitu vinatawanyika,

Upepo una kadhia!38

Pacha wa maji ni moto,

Mithili Kurwa na Doto,

Maji yakosapo joto,

Moto yanayazimua.39

Jua hili liwakalo,

Kila twendapo tunalo,

Mwanga utupatialo,

Ni uhai wa Dunia.

40

Pale Jua likizama,

Mwezi nao huandama,

Usiku hujaa neema,

Kwa mwanga ulotulia,41

Mbinguni kwameremeta,

Kulivyoenea nyota,

Kwa macho ukizifwata,

Mwishowe utasinzia.

42

Hizo sayari za juu,

Wataenda vitukuu,

Sisi wa muhula huu,

Wajibu kuwaandaa.

III. Taswira ya Ulimwengu

43

Ulimwengu ni mpana,

Tanzania hadi China,

Twaishi kwa kupishana,

Kufa ni kutangulia.44

Idadi ya wanadamu,

Ni kubwa kitarakimu,

Wakuko kila sehemu,

Duniani wamejaa.45

Dunia na matatizo,

Ndio chanzo cha mizozo,

Izushayo magumzo,

Watu wakahadithia.46

Dunia ni kila mtu,

Kuanzia wenye vitu,

Na waonwao sio kitu,

Wote ni wake raia.47

Yenye waja madhalimu,

Wapendao kudhulumu,

Wahujumuo kaumu,

Kwa kula kwa kufakia.

48

Dunia hii ya visa,

Vinavyoleta mikasa,

Tangu kale hadi sasa,

Bado hakujatulia.49

Dunia ya ubaguzi,

Ulojaa uchochezi,

Wazawa na walowezi,

Hawaja swarifu nia.50

Rangi nayo ni balaa,

Kwa wale ilo zingia,

Wageuzwao kinyaa,

Utu wao kupotea.51

Hudhalilishwa ubongo,

Kuchoshwa kila kiungo,

Ukaenezwa uongo,


Purchase this book or download sample versions for your ebook reader.
(Pages 1-16 show above.)